Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi ya Paris

Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi ya Paris

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea muda mfupi uliopita kwenye maeneo kadhaa mjini Paris Ufaransa.

Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Ban ametoa wito watu ambao bado wametekwa nyara kwenye ukumbi wa muziki wa Bataclan waachiliwe huru mara moja.

Aidha amesema anaamini kwamba mamlaka za serikali ya Ufaransa zitafanya lolote liwezekanalo ili kupeleka watekelezaji wa uhalifu huo mbele ya sheria.

Katibu Mkuu ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga akiwatakia nafuu waliojeruhiwa, huku akielezea mshikamano na serikali na raia wa Ufaransa.

Wakati huo huo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia rais wake Morgens Lykeketoft, limelaani shambulizi hilo na kusema dunia nzima inachukizwa na kitendo hicho.

Katika taarifa yake ameelezea mshikamano na Ufaransa na raia wake na kusisitiza kuwa ugaidi na mauaji ya aina hiyo ni uhalifu wa kibinadamu.

Amesema ulimwengu unapaswa kuwa na msimamo mmoja juu ya uhalifu wa aina hiyo usio na nafasi katika zama za sasa.