Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapalestina na Waisraeli wahitaji matumaini ya amani: Eliasson

Wapalestina na Waisraeli wahitaji matumaini ya amani: Eliasson

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala maalum kuhusu Mashariki ya Kati wakati ambapo vurugu zinazidi kuongezeka baina ya Palestina na Israel.

Akiongea wakati wa mkutano huo, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema ni muhimu kurejesha matumaini ya amani kwa wapalestina na waisraeli, kwa sababu mzozo huo umefikia hatua hatarishi kabisa.

Bwana Eliasson ameongeza kwamba hakuna sababu yoyote inayoweza kueleza mashambulizi makali dhidi ya raia na vitendo vya ugaidi.

Akikaribisha jitihada za polisi wa Israel na Palestina kuimarisha mifumo ya ulinzi wa usalama, Bwana Eliasson amesisitiza umuhimu wa suluhu ya kisiasa

(Sauti ya bwana Eliasson)

« Hata kama ni muhimu, harakati za usalama pekee yake hazitatosha. Mzozo haungetokea iwapo raia wa Palestina wangekuwa na matumaini ya kuwa na taifa lao wenyewe. Kwa kifupi iwapo wapalestina wangekuwa hawaishi kwenye hali ya kunyanyaswa na kudharauliwa katika utawala uliodumu kwa karibu miaka 50. »

Hatimaye amesisitiza umuhimu wa kuimarisha taasisi za Palestina sambamba na mazingira ya kiuchumi.