Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani shambulizi la bombu msikitini, Yemen

Baraza la Usalama lalaani shambulizi la bombu msikitini, Yemen

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamelaani vikali mashambulizi ya bomu ya Septemba 24 kwenye msikiti mjini Sana’a, Yemen, ambalo lilisababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi.

Katika taarifa, wajumbe hao wamepeleka ujumbe wa kuomboleza na rambirambi kwa familia na marafiki wa waliouawa na mejeruhi katika vitendo hivyo viovu, pamoja na kwa watu na serikali ya Yemen.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamekariri kuwa aina zote za ugaidi ni moja ya matishio makubwa zaidi kwa amani na usalama wa kimataifa, na kwamba vitendo vyovyote vya kigaidi ni uhalifu usiokubalika, bila kujali kichochezi, wapi vinafanyika, lini, na nani anayevifanya.

Aidha, wajumbe hao wamekariri ari yao kukabiliana na aina zote za ugaidi, kulingana na wajibu wao chini ya katiba ya Umoja wa Mataifa, na kusisitiza haja ya kuwafikisha watendaji, waandaaji na wafadhili wa vitendo hivyo mbele ya sheria, na kuzihimiza nchi zote kushirikiana na mamlaka za Yemen kuhusu suala hili, kulingana na wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama.