Skip to main content

WHO yawaenzi wahudumu wa afya kwenye Siku ya Kibinadamu

WHO yawaenzi wahudumu wa afya kwenye Siku ya Kibinadamu

Katika kuelekea Siku ya Kibinadamu Duniani, Shirika la Afya Duniani, WHO, linamulika mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wahudumu wa afya na miundombinu ya afya, ambayo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt. Margaret Chan, ametaja kuwa ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Katika mchakato wa kuwaenzi wahudumu wa afya, WHO itazindua kampeni kwenye intaneti ya kutambua juhudi za madaktari, wauguzi na wahudumu wengine, na kukumbusha nchi wanachama na pande kinzani katika mizozo kutimiza wajibu wao wa kuwalinda wahudumu wa afya na mfumo mzima wa huduma za afya.

Kampeni hiyo inalenga kumulika hatari zinazowakabili wahudumu wa afya na haja ya kuongeza juhudi za kuwalina.

Mnamo mwaka 2015, mamia ya wahudumu wa afya wamefariki dunia katika maeneo ya migogori na wakati wakipambana na milipuko ya magonjwa kama vile Ebola. Daktari Rudy Coninx ni mtalaam wa maswala ya dharura na ya kibinadamu wa WHO

“ Leo Ebola ikikaribia kutokomezwa, naamini kwamba tumepata visa vitatu tu wiki hii, ni kwa sababu ya wahudumu wa afya. Lakini wanafanya hivyo kwa kuweka maisha yao hatarini sana. Wahudumu wa afya 875 wameambukizwa ugonjwa wa Ebola na karibu nusu yao wamefariki dunia.”