Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yaadhimisha mwaka mmoja bila Polio

Somalia yaadhimisha mwaka mmoja bila Polio

Somalia imeadhimisha mwaka mmoja bila ripoti ya kisa kipya cha Polio kwa tukio maalum la utolewaji wa chanjo kwa watoto walio chini ya miaka mitano katika kambi kubwa kabisa ya wakimbizi wa ndani mjini Mogadishu.

Tukio hilo limehudhuriwa na waziri wa afya wa Somalia na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa balozi Nicholas Kay, mwakilishi mkazi na mratibu wa misaada ya kibinadamu Peter de Clercq pamoja na mwakilishi wa shirika la afya ulimwenguni WHO.

Akizungumza katika utolewaji wa chanjo mwakilishi wa WHO nchini humo Dr Ghulam Popal amesema wakati taifa likisisimka kwa mafanikio hayo ni muhimu kuendeleza juhudi za utolewaji wa chanjo na kuongeza bidi ili kuyafikia maeneo ambayo bado hayajafikiwa.

Kwa upande wake mratibu mkazi  wa misaada ya kibinadamu  Peter de Clercq amesema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za zaidi ya Wasomali 10,000 waliojitolea na wafanyakazi wa afya ambao walitoa chanjo kwa watoto zaidi ya milioni mbili walio chini ya umri wa miaka mitano kwa kutembelea kila kaya nchini Somalia.