Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Warundi zaidi ya 20,000 wakimbilia Rwanda

Warundi zaidi ya 20,000 wakimbilia Rwanda

Maandamano yameanza jumapili, tarehe 26 mjini Bujumbura, nchini Burundi, baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumteua rais Pierre Nkurunziza kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa rais wa mwezi Juni, ikiwa ni awamu ya tatu.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA imesema kwamba watu watano wanadaiwa kuuawa tangu jumapili, na kuna ripoti pia za kutishia vyombo vya habari na kufungwa kwa wawakilishi wa upinzani.

Kwa mujibu wa Shirila la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR nchini Rwanda, ni watu 20,408 kutoka Burundi ambao wamesaka hifadhi Rwanda kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Shirika hilo limetangaza kufunguliwa kwa kambi mpya ya wakimbizi mjini Mahame, kwa ushirikiano na serikali ya Rwanda, huku idadi ya wakimbizi inayofika mpakani kila siku ikiongezeka kwa kasi.

Halikadhalika, watu 4,000 wametafuta hifadhi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na wengine 100 nchini Tanzania.

Wadau mbali mbali wakiwemo kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa wameonya kwamba kugombea kwa awamu ya tatu kwa rais Pierre Nkurunziza ni kinyume na sheria ya kikatiba na makubaliano ya Amani na Maridhiano ya Arusha ya mwaka 2000.