Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani uharibifu wa Nimrud, Iraq

UNESCO yalaani uharibifu wa Nimrud, Iraq

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO Irina Bokova amelaani vikali uharibifu uliofanywa na magaidi dhidi ya eneo la makumbusho ya kale huko Nimrud nchini Iraq.

Katika taarifa yake amesema uharibifu huo wa makusudi unaoonyeshwa kupitia video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii unadhihirisha tu siyo kwamba magaidi wanalenga vilivyomo ndani yake bali pia wanataka kufuta historia nzima ya wananchi wa Iraq.

Ameelezea mshikamano wake na wananchi na serikali ya Iraq na kurejelea hatua za UNESCO za kulinda urithi wa maeneo na kuratibu jitihada za jamii ya kimataifa dhidi ya usafirishaji haramu wa mali za kitamaduni.

Bi. Bokova amesema uharibifu wa makusudi wa urithi ni uhalifu wa kivita akisema watafanya kila wawezalo kukabiliana na jambo hilo ikiwemo kuhifadhi kumbukumbu husika ili watuhumiwa waweze kufikishwa mbele ya sheria.

Nimrud ilishambuliwa tarehe Sita mwezi uliopita na video ya hivi karibuni inaonyesha uharibifu kabisa wa upande wa Kaskazini-Magharibi wa kasri ya Ashurnasirpal wa II iliyojengwa miaka ya 879 kabla ya Kristo.