Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Krahenbuhl aingia siku ya pili ya ziara yake Yarmouk:

Krahenbuhl aingia siku ya pili ya ziara yake Yarmouk:

Ziara ya Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA Pierre Krahenbuhl kwenye kambi ya Yarmouk nchini Syria imeingia siku ya pili leo ambapo amesisitiza umuhimu wa kuangalia njia za kuwapatia misaada ya kibinadamu wakimbizi hao walionaswa kwenye taabu.

UNRWA imesema tayari akiwa kwenye ziara hiyo aliyoiita kuwa ni ya dharura, amekuwa na mazungumzo na maafisa wa serikali ya Syria inayotia moyo juu ya kurejesha hali ya matumaini kwa wakimbizi hao wa kipalestina lakini amesema bado kuna mengi ya kufanya ambapo leo anakuwa na mazungumzo na maafisa waandamizi juu ya kufikisha misada hiyo.

Bwana Krahenbuhl amesema ameguswa zaidi na simulizi za wakimbizi waliokimbia kambi ya Yarmouk na sasa wanaishi umbali wa mita 200 nje ya kambi hiyo akitolea mfano mama mmoja aliyelazimika kukimbia mapigano akiwa na mwanae aliyekuwa na umri wa siku moja.

Kamishna huyo mkuu wa UNRWA amesema janga la Syria lina mtazamo wa kibinadamu na hivyo harakati za kushughulikia janga hilo ni lazima zipatie kipaumbele utu na heshima ya raia.

Kambi ya Yarmouk iko kusini mwa mji mkuu wa Syria, Damascus na ni imekuwa ikihifadhi wakimbizi zaidi ya 200,000 wa kipalestina waliokimbia mzozo huko Palestina, hata hivyo hivi sasa wengi wao wamekimbia kambi hiyo kutokana na mapigano nchini Syria.