Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wameuawa na mabomu ya kutegwa ardhini Ukraine

Watoto wameuawa na mabomu ya kutegwa ardhini Ukraine

Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesema kuwa watoto wapatao 109 wameripotiwa kujeruhiwa huku wengine 42 wakiuawa na mabomu ya kutegwa ardhini na mabomu vilipuzi ambavyo havikulipuka katika maeneo ya Donetsk na Luhansk, mashariki mwa Ukraine tangu Machi mwaka 2014.

Mwakilishi wa UNICEF ukanda wa Kati na Mashariki mwa Ulaya, Marie Pierre Poirier, amesema idadi hiyo huenda ikawa juu zaidi iwapo yatajumuishwa maeneo yasiyodhibitiwa na serikali, akiongeza kuwa wadau wa kibinadamu wanapata ugumu kuyafikia maeneo hayo, ambayo ni changamoto kubwa. UNICEF na wadau wake wamezindua kampeni ya kupunguza hatari za mabomu ya kutegwa ardhini, ili kuwapa watoto na familia zao taarifa muhimu kuhusu hizo hatari.

Christophe Boulierac ni msemaji wa UNICEF, Geneva.

"Kampeni hii inajumuisha ujumbe wa kuelimisha wa maandishi, video na njia ya dijitali, pamoja na kuwapa mafunzo walimu 100 na watoa ushauri nasaha shuleni kuhusu hatari za mabomu ya ardhini. Ikiwa ni siku chache kabla siku ya kimataifa ya kuhamasisha kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini mnamo Aprili 4, hali nchini Ukraine ni kumbusho kuwa licha ya hatua zilizopigwa duniani kuondoa mabomu ya ardhini, watoto na jamii bado wanaendelea kuwa wahanga wa mabomu hayo na vilipuzi vya mabaki ya vita.”

Kufikia sasa, UNICEF na wadau wametambua na kuondoa zaidi ya mabomu na vilipuzi 33,717 kutoka Donetsk na Luhansk.

Watu wapatao milioni 5 nchini Ukraine wameathiriwa na mzozo unaoendelea, milioni 1.1 wakiwa wamelazimika kuhama makwao ndani ya nchi.