Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa kubaki Afghanistan mwaka mmoja mwingine

Umoja wa Mataifa kubaki Afghanistan mwaka mmoja mwingine

Leo Baraza la usalama kwa kauli moja limepitisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan(UNAMA) kwa mwaka mmoja wa ziada.

Akihutubia Baraza hilo kuhusu mwelekeo wa kisiasa nchini humo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa UNAMA, Nicholas Haysom amesema matumaini ya maridhiano na amani yapo nchini humo.

Amekaribisha jitihada zinazofanywa na rais mpya Ashraf Ghani na Ofisa Mtendaji wake Abdullah Abdullah katika kuunda serikali jumuishi, baraza zima la mawaziri likiwa bado halijatangazwa. Aidha amewapongeza kwa kuanza utaratibu wa maridhiano na waasi wa Taliban.

(Sauti ya Nicholas Haysom)

“ Amani ndilo suluhu pekee kwa  Afghanistan. Na ushindi wa kijeshi si suluhu bora kwa utangamano wa kudumu wa jamii. Amani ya kudumu inahitaji utaratibu jumuishi utokanao na  msingi wa mafanikio yaliyopatikana Afghanistan katika muongo uliopita. "

Halikadhalika bwana Haysom amesema bado ni lazima kuimarisha hali ya demokrasia na sheria ya uchaguzi, wakati ambapo uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa unatakiwa kufanyika mwaka huu.

Mkuu wa UNAMA ameeleza wasiwasi wake juu ya haki za binadamu nchini humo, akilikumbusha Baraza la Usalama kwamba raia 10,000 wamejeruhiwa au kuuawa mwaka 2014 kutokana na mapigano.

Hatimaye, amepeleka salamu zake za rambirambi kwa wahanga 200 wa mafuriko yaliyotokea hivi karibuni nchini humo, akisema majanga hayo yanaonyesha kuwa nchi hiyo haikumbwi tu na shida za usalama bali pia matatizo ya kibinadamu.