Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi ya Gbagbo na Blé Goudé kusikilizwa pamoja- ICC

Kesi ya Gbagbo na Blé Goudé kusikilizwa pamoja- ICC

Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai, ICC, leo imempa Mwendesha Mashtaka Mkuu idhini ya kuziunganisha kesi za aliyekuwa rais wa Cote d’Ivoire, Laurent Gbagbo na Charles Blé Goudé, ili kuwezesha kuharakisha kuendeshwa kwa mashtaka dhidi yao.

Mahakama hiyo pia imehamisha tarehe ya kuanza kuisikiliza kesi ya Gbagbo kutoka Julai 5, 2015 na kuirudisha nyuma hadi  Aprili 21, 2015 watakapofikishwa washukiwa mahakamani ili kutathmini masuala ya kitaaluma yanayohusiana na kesi hiyo.

Mahakama hiyo imezingatia kuwa Bwana Gbagbo na Blé Goudé wamethibitishiwa mashtaka dhidi yao, ambayo yanatokana na madai yanayosawiana, yakiwa ni madai ya uhalifu unaoshukiwa kuutekelezwa katika matukio manne na washukiwa wale wale, ambao waliwalenga wahanga wale wale kwa sababu walionekana kuwa wafuasi wa Alassane Ouattara.

Mahakama imesema kuwa ingawa madai ya kushiriki kwao na mchango wao katika kuandaa na kutekeleza mpango wa uhalifu huo hakusawiani, vitendo vya Bwana Gbagbo na Blé Goudé vilihusiana kwa karibu.