Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Asia Pasifiki zapaswa kutahadhari zaidi majanga yanapozidi kutokea

Nchi za Asia Pasifiki zapaswa kutahadhari zaidi majanga yanapozidi kutokea

Mwaka 2014, zaidi ya nusu ya majanga yametokea katika ukanda wa Asia na Pasifiki, yakisababisha vifo 6,000 kwenye ukanda huo.Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya tume ya uchumi na kijamii kwenye ukanda wa Asia Pasifiki, ESCAP iliyotolewa leo.

ESCAP imesema, mvua na mmomonyoko wa ardhi ni chanzo cha asilimia 85 ya majanga yaliyotokea na kwa ujumla, matukio haya yameathiri takriban watu milioni 80 kwenye ukanda huo.

Changamoto kubwa, kulingana na takwimu za ripoti ya ESCAP ni uthabiti wa mfumo wa kiuchumi, hasara za kiuchumi zikifikia dola bilioni 59.

Hatimaye tume hiyo ya kimataifa imesisitiza umuhimu wa nchi za Asia Pasifiki kujitayarisha awali, kwani majanga kama hayo yatazidi kutokea kulingana na mabadiliko ya tabianchi. ESCAP imesema cha msingi ni kufanya maandalizi mapema ili kuwa na mfumo kamilifu wa kupata taarifa, kutahadhari, na kuhamisha watu wakiwa hatarini, pamoja na ushirikiano wa kimataifa.