Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kobler asikitishwa na mashambulizi mjini Aru, DRC

Kobler asikitishwa na mashambulizi mjini Aru, DRC

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, DRC, na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, Martin Kobler, ameeleza kusikitishwa sana na mashambulizi dhidi ya raia wa Aru, katika jimbo la Ituri, mashariki mwa DRC.

Kwa mujibu wa Radio Okapi ya MONUSCO, mashambulizi hayo yametokea Jumamosi usiku kwenye klabu, ambapo watu walikuwa wanasherehekea ushindi wa timu ya taifa katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika.

Watu 15 wamefariki dunia, akiwemo mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa, na wengine 17 wamejeruhiwa.

Martin Kobler, pamoja na viongozi wa serikali ya jimbo hilo, amewatembelea majeruhi hospitalini, akiwatakia nafuu na kupeleka salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga.