Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumakinike Polio isiibuke tena Mashariki ya Kati:Wataalamu

Tumakinike Polio isiibuke tena Mashariki ya Kati:Wataalamu

Huko Mashariki ya kati kuna habari njema kuwa huduma ya dharura ya chanjo ya polio iliyofanyika mwa miezi 12 inaonekana kusitisha kuzuka kwa ugonjwa huo ulioanzia  Syria na Iraq. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya

(TAARIFA YA GRACE)

Mlipuko huo ulisababisha kupooza kwa watoto wapatao 38 nchini Syria na Iraq na kusababisha hofu ya janga kubwa, ambapo kampeni iliwezesha chanjo dhidi ya polio kwa watoto zaidi ya milioni 27 katika nchi 8.

Taarifa ya pamoja ya WHO na UNICEF imesema mwaka mmoja sasa umepita tangu kuthibitishwa kwa kisa cha Polio huko Syria, na miezi tisa tangu kuripotiwa kwa kisa cha mwisho nchini Iraq, licha ya mgogoro unaoendelea na kufurushwa kwa watu kutoka makwao katika ukanda huo.

Hata hivyo wanaonya kuwa mafanikio hayo yanaweza kutoweka kwani mapigano yanayoendelea Syria na Iraq, yanatishia baadhi ya watoto wasifikiwe na huduma ya chanjo mara kwa mara.