Waasi Sudan Kusini waanza kuachilia huru watoto wanaowatumikisha: UNICEF

27 Januari 2015

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake wamefanikisha mpango wa kuachiliwa huru kwa watoto wapatao 3,000 wanaotumikishwa na vikundi vilivyojihami nchini Sudan Kusini, ikieleza kuwa hiyo ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufikia hatua hiyo. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

UNICEF inasema tayari kundi la kwanza la watoto 280 wameachiliwa huru leo Jumanne kwenye kijiji cha Gumuruk jimbo la Jonglei, Mashariki kwa Sudan Kusini.

Mwakilishi wa UNICEF Sudan Kusini Jonathan Veitch amesema makubaliano ni kuwa watoto hao wenye umri wa kati ya miaka 11 hadi 17 wataachiliwa huru taratibu ambapo wengine watakabidhiwa mwezi ujao.

Watoto hao wametumikishwa na waasi wa South Sudan Democratic Army (SSDA) Cobra kinachoongozwa na David Yau Yau.

Christophe Boulierac ni msemaji wa UNICEF.

Wanahitaji msaada wa muda mrefu ili kuunganishwa tena. Wengi hawajawahi kwenda shuleni. Wanaweza kukabiliwa na matatizo mengi wakati wa kujumuishwa katika jamii na familia zao. Baadhi yao wamepigana kwa miaka minne. Kwa hiyo utaratibu huu utakuwa mrefu na wenye changamoto nyingi. Kuna hatari kwa watoto hao kukabiliana na ubaguzi, kuna hatari pia ya kurudi vitani. 

Watoto hao walisalimisha silaha na sare zao kwenye hafla iliyofadhiliwa na UNICEF na kushuhudiwa na ujumbe kutoka Tume ya Sudan Kusini ya upokonyaji silaha waasi na ujumuishaji wapiganaji kwenye jamii na wale wa kikundi hicho cha SSDA-Cobra.

Kwa mujibu wa UNICEF gharama ya mtoto mmoja kuachiliwa huru na waasi hao na hatimaye kujumuishwa katika jamii ni takribani dola 2,330 kwa mwaka mmoja.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter