Sri Lanka isitishe ghasia kwa msingi wa kidini: UM waomba

2 Julai 2014

Wataalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kuwa na dini na kuhusu masuala ya walio wachache wameiomba leo serikali ya Sri Lanka kuchukua hatua ili wasitishe ghasia zinazotekelezwa na vikundi vya wafuasi wa Budha wenye msimamo mkali dhidi ya jamii za Wakristo na za Waislamu. Wameomba wapelekwe mbele ya sheria.

Zaidi ya visa 350 vya mashambulizi dhidi ya Waislamu na zaidi ya visa 150 dhidi ya Wakristo vimeripotiwa Sri Lanka kwa kipindi cha miaka miwili, jamii hizo zikikumbwa na ubaguzi na maneno ya chuki pia.

Tarehe 15, Juni, watu wanne walifariki dunia baada ya maandamano ya kundi moja la wafuasi wa Budha wenye msimamo mkali.

Heiner Bielefeldt, ambaye ni Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kuwa na imani au dini, amesema ghasia zinaendelea kwa sababu ya hali ya ukwepaji wa sheria iliyomo Sri Lanka, akitoa wito kwa Sri Lanka kuhakikisha kuwepo kwa haki ya kuwa na dini kwa walio wachache na kusitisha maneno ya chuki kwa msingi wa kidini.

Vikundi hivyo vya kidini vyenye msimamo mkali wanaamini kwamba wafuasi wa Budha ni watu wa aina nzuri zaidi kuliko wote, wakisambaza majungu kuhusu jamii za Wakristo na Waislamu, ili kutisha wenzao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud