Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali nchini Mali yamulikwa katika Baraza la Usalama

UN Photo.
Baraza la Usalama.

Hali nchini Mali yamulikwa katika Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na mashauriano kuhusu hali nchini Mali, likihutubiwa na Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani, Hervé Ladsous na Mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Mali, Albert Koenders.

Kikao hicho kimetoa fursa kwa wanachama wa Baraza hilo kujadili kuhusu ripoti ya Katibu Mkuu ya Juni 9 mwaka huu, na mapendekezo yake kuhusu kuongezwa kwa muda na mamlaka ya Ujumbe Mseto wa Kuweka Utulivu nchini Mali, MINUSMA.

Inatarajiwa kuwa azimio la kuongeza muda na mamlaka ya MINUSMA, litapitishwa wiki ijayo.

Akizungumza mbele ya baraza la usalama leo, Herve Ladsous ameelezea zaidi kuhusu hali iliyopo hivi sasa nchini Mali:

“ Licha ya jitihada za jamii ya kimataifa na mamlaka za Mali, tumeona kwamba mauaji yaliyotokezea Kidal na matokeo yake, pamoja na ukosefu wa usalama uliosababishwa na kuwepo kwa vikundi vya wagaidi kaskazini mwa Mali, hayo yote yanaonyesha kazi zilizopo mbele yetu ili tufikie hali ya utulivu wa kudumu.”

Halikadhalika, Ladsous ametoa wito kwa wadau wote kufikia suluhu ya kudumu, akisema:

“ Hatuwezi kuendelea na hii hali. Lazima tuendeleze kwa haraka utaratibu wa kisiasa. Muda wa mazungumzo ya amani umefika sasa !”