Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kinachoendelea Ukraine kinasikitisha: Feltman

Kinachoendelea Ukraine kinasikitisha: Feltman

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana tena kwa mara nyingine kujadili hali inavyoendelea nchini Ukraine ambapo wajumbe wameelezwa bayana kuwa matukio ya siku nne zilizopita yanapaswa kuwa kiashirio ya kwamba hatua za dharura zinahitajika.

Picha halisi ya matukio hayo imeelezwa na Mkuu wa masuala ya siasa ndani ya Umoja huo Jeffrey Feltman ambaye ameyataja kuwa ni pamoja na kutekwa kwa waangalizi kutoka shirika la usalama na ushirikiano la Ulaya-OSCE, kundi la wanaotaka kujitenga kujichukulia majengo ya serikali na kupigwa risasi kwa meya wa mji mmoja wa mashariki nchini Ukraine.
Amesema matarajio ya amani yaliyodhihirishwa tarehe 17 Aprili kutokana na mazungumzo ya Geneva yametoweka na utekelezaji wa tamko la Geneva umekwama kutokana na kila pande kuibuka na tafsiri yake akiongeza kuwa tambo kutoka pande kinzani kwenye mzozo huo zimekuwa hazina msaada wowote.
Bwana Feltman amesema hali inazidi kuzorota…..
(Sauti ya Feltman)
“Wakati huo huo hali katika baadhi ya sehemu mashariki mwa Ukraine inazidi kuzorota. Tarehe 25 mwezi Aprili kundi la waangalizi wa kutoka OSCE walikamatwa na kushikiliwa. Ijapokuwa mmoja wao ameachiwa huru, wengine bado wanashikiliwa.
Amerejelea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon wa kulaani tukio hilo na kusihi wahusika wawaachie huru wanaoshikiliwa bila masharti yoyote na bila kuwajeruhi.
Halikadhalika amesihi wale wenye ushawishi na pande husika katika mzozo kusaidia ili kupata suluhu haraka kwani uhai uko hatarini.