Pillay ataka pande zinazopigana Sudan Kusini kujali maisha ya raia

24 Disemba 2013

Kamishna wa Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay amezitaka mamlaka zinazohusika katika mzozo wa Sudan Kusini kujiepusha na matumizi zaidi ya nguvu katika wakati ambapo taarifa zinasema kuwa mamia ya raia wameathiriwa zaidi baada ya mapigano hayo kuingia siku ya kumi.

Pillay amesema binafsi imeingia na wasiwasi mkubwa kutokana na machafuko hayo yanavyoendelea kuchukua mkondo wa hatari kwa raia wasiokuwa na hatia na amewataka wahusika wake kutafakari mara mbili.

Amesema machafuko hayo sasa yanabeba sura ya kikabila jambo ambalo kama halitadhibitiwa sasa linaweza kuvuruga kabisa majaliwa ya taifa hilo lilijitenga kutoka Sudan na kuwa taifa jipya barani Afrika.

Kamishna huyo ameelezea pia wasiwasi wake kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama hata kwa makundi ya raia yaliyoomba hifadhi kwenye kambi za Umoja wa Mataifa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud