Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zambia yaingia kipindi muhimu katika vita dhidi ya Ukimwi

Zambia yaingia kipindi muhimu katika vita dhidi ya Ukimwi

Shirika la Umoja wa Mataifa linaohusika na mapambano dhidi ya Ukimwi, UNAIDS limesema Zambia iko katika hatua muhimu zaidi dhidi ya ugonjwa huo ambapo limesema nchi hiyo haipaswi kubweteka na mafanikio ilipata.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS Jan Beagle amesema hayo mwishoni mwa ziara ya siku tatu ya ujumbe alioongoza kwenye nchi hiyo ambako takribani asilimia 13 ya watu wazima wanaishi na virusi vya Ukimwi.

Amesema kumekuwepo na mafanikio kwenye kupunguza maambukizi mapya kwa watoto na hata upatikanaji wa tiba dhidi ya magonjwa nyemelezi lakini bado kuna maambukizi mapya miongoni mwa vijana, kasi ndogo ya upimaji na ukosefu wa huduma kwa makundi muhimu.

Ukiwa Zambia, ujumbe huo uliojumuisha pia wajumbe kutoka Australia,Brazil, India, Norway, Poland na Zimbabwe ulipata fursa ya kuzungumza na Makamu wa Rais na viongozi wa ngazi za juu pamoja na wawakilishi wa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Halikadhalika walishiriki jumuiko la kitaifa kuhusu kinga dhidi ya Ukimwi ambapo Makamu wa Rais alizungumzia dhima ya viongozi wa kijadi na machifu katika kushawishi jamii kubadili mienendo na tabia.