Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu Maalum wa UM-OPCW atoa taarifa kwa Baraza la Usalama

Mratibu Maalum wa UM-OPCW atoa taarifa kwa Baraza la Usalama

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limepata taarifa ya Katibu Mkuu kuhusu Syria ambapo pamoja na mambo mengine inaelezea kazi ya uteketezaji wa mpango wa silaha za kemikali nchini Syria, kazi inayofanywa kwa pamoja na umoja huo na shirika la kimataifa linalopinga matumizi ya silaha hizo, OPCW.

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo na kufanya mashauriano ya faragha, mratibu maalum wa ujumbe huo Sigrid Kaag alizungumza na waandishi wa habari na kuwaelezea kwa muhtasari kuwa wajumbe walikuwa na tashwiswhi ikiwemo usalama wa watendaji ……

“Tulikuwa na mjadala mzuri sana na wajumbe wa baraza, maswali yaliibuka kuhusu usalama wa watendaji, majukumu tarajiwa ya ujumbe huu wa pamoja bila shaka kuendelea kuthibitisha na kufuatilia, lakini pia utekelezaji wa awamu ya tatu itakapokubaliwa. Na kwa ujumla maswali kuhusu maeneo mawili ambayo hatukuweza kutembelea, lakini yalikuwa yametelekezwa kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Syria kwa OPCW. Na kama tulivyozingatia kwenye vyombo vya habari, azma ni kutembelea siku za usoni kwa kuzingatia hali ya usalama nchini humo.”

Kuhusu eneo ambako silaha za kemikali zitateketezwa, Bi. Kaag amesema mashauriano yanaendelea huko The Hague kati ya mamlaka za Syria, Umoja wa Mataifa na OPCW. Tayari Mkurugenzi Mkuu wa OPCW Ahmet Üzümcü, alieleza bayana kuwa Syria inataka uteketezaji huo ufanyike maeneo mengine kutokana na mzozo wa kivita nchini humo.