UNHCR yahofia hatma ya mkimbizi wa Rwanda Joel Mutabazi

5 Novemba 2013

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR latiwa wasiwasi na hali ya Joel Mutabazi, mkimbizi wa Rwanda aliyekamatwa na kukabidhiwa kwa serikali ya nchi yake na polisi wa Uganda bila ridhaa yake mnamo Jumamosi ya oktoba 26 mwaka huu.

Waziri wa Uganda anayehusika na masuala ya wakimbizi amethibitishwa kukamatwa na kukabidhiwa kwa mkimbizi huyo na kujutia kwamba hicho kilikuwa ni kitendo cha makosa kwa maafisa waliotekeleza zoezi hilo.

Pia ametangaza kusitishwa kazi kwa maofisa waliofanya kitendo hicho wakati uchunguzi ukiendelea kubaini nini kilichotekea na kwamba kukmabidhi bwana Mutabazi hakutoathiri jukumu la Uganda la kulinda wakimbizi chini ya sheria za kimataifa za wakimbizi na zile za Uganda pia.

UNHCR inashukuru kwa hatua hizo zilizochukuliwa na serikali , lakini imeshangazwa na kushitushwa kwamba ukiukwaji mkubwa wa jukumu la kulinda umetekelezwa na vyombo vya dola na kumuweka bwana Mutabazi hatarini.

Shirika hilo limesema linasubiri kwa hamu uchunguzi ulioahidiwa na waziri wa masuala ya wakimbizi na likitumai utafanyika kwa haraka na kwa uwazi ili waliohusika waweze kuwajibishwa. UNHCR inaendelea kuhofia usalama wa bwana Mutabazi na umeitaka serikali ya Rwanda kuheshimu haki zake za binadamu na za kisheria.