Tunalaani vikali shambulizi kwa msafara wa harusi Nigeria: UN OHCHR

5 Novemba 2013

Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imelaani vikali shambulizi  dhidi ya msafara wa harusi lilitokea kwenye jimbo la Borno nchini Nigeria mwishoni mwa wiki. Mnamo tarehe 2 mwezi huu watu 30 waliokuwa wakihudhuria harusi walitekwa na kuawa kwenye barabara ya Bama-Mubi-Banki  jimbo la Borno.

Barabara hiyo iko karibu na mapaka na Cameroon na huwa ina visa vingi vya uvamizi kutoka kwa kundi la Boko Haram. Wakati wa shambulizi hilo wanajeshi wanne waliuawa huku daraja linalounganisha mji ulio karibu likilipuliwa.

Kulingana na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kunashuhudiwa mashambulizi karibu kila siku kaskazini Mashariki mwa Nigeria hasa jimbo la Borno na maeneo yaliyo karibu. Cecile Poully ni msemaji wa Ofisi ya haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Tunalaani vikali mashambulizi ya Boko Haram ambao wanaendelea kuwalenga raia wakiwemo wanafunzi, waumini , wanasiasa maafisa wa serikali, wageni na pia wanajeshi. Wanachama wa Boko Haram na makundi mengine ikiwa watahukumiwa kwa kuendesha mashambulizi dhidi ya raia na pia dhidi  ya dini na makabila watapatikana na mokosa ya uhalifu dhidi ya binadamu.”