Baraza la Usalama laangazia ushirikiano wa UM na Muungano wa nchi za Kiislamu

28 Oktoba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao cha ngazi ya juu kuhusu ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Nchi za Kiislamu, OIC. Joshua Mmali amekifuatilia kikao hicho:

Kikao cha leo katika Baraza la Usalama kimehudhuriwa na kuhutubiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, na Katibu Mkuu wa Muungano wa Nchi za Kiislamu, OIC, Bwana Ekmeleddin İhsanoğlu.

Katika hotuba yake, Bwana Ban amesema changamoto za amani na usalama zilizopo sasa ni sugu mno, na hakuna nchi au shirika moja lenye uwezo wa kukabiliana nazo peke yake. Bwana Ban ameongeza kuwa ili kupata ufanisi, juhudi na mikakati ya pamoja inahitajika.

“Umojwa wa Mataifa unashirikiana na OIC kuhusu masuala mengi yakiwemo kuzuia migogoro na kukabiliana na ugaidi, haki za binadamu na masuala ya kibinadamu, na pia mazungumzo baina ya tamaduni tofauti na maendeleo endelevu. Kuhusu Syria, tunaendelea kushirikiana katika juhudi za kibinadamu na kisiasa.”

Naye rais wa OIC, Ekmeleddin İhsanoğlu, ameunga mkono kauli ya Bwana Ban kuhusu mtazamo wake wa ushirikiano huo

“Kwa upande wetu, tunaazizia mno ushirikiano wetu na Umoja wa Mataifa, na tupo tayari kujenga ushirikiano wa dhati ili kuendeleza amani, sheria, haki za binadamu na maendeleo.”