Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majaji ICC watoa mwongozo kuhusu kesi ya Ruto na mwenzake

Majaji ICC watoa mwongozo kuhusu kesi ya Ruto na mwenzake

Majaji wanaohusika na rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC, wamekataa ombi la makamu wa rais wa Kenya, William Ruto, la kutaka kuruhusiwa kutohudhuria vikao vya kesi inayomkabili.

Pia majaji hao wametasfiri vifungu vya sheria vinavyoweza kutoa ruhusa kwa mshtakiwa kutokuwepo mahakani wakati wa kesi yake.

Taarifa zaidi na George Njogopa

Ruto  anayeshtakiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, aliwataka majaji wa Mahakama ya ICC iliyoko The Hague, Uholanzi, kumruhusu ahudhurie tu vikao vya mwanzo na mwisho vya kesi yake.

Uamuzi huo wa ICC utakuwa unatofautiana na serikali ya Kenya na Umoja wa Afrika ambao ulitaka kesi dhidi ya Ruto na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ihamishiwe karibu na nyumbani au iahirishwe kabisa

Rufani ya Ruto ambaye ni Makamu wa Rais wa Kenya, ilipata uungwaji mkono toka kwa mataifa jirani ikiwemo Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda ambayo yaliwasilisha hoja binafsi kwenye mahakama hiyo.

Akisoma uamuzi wa majaji juu ya rufani hiyo, Rais wa Majaji hao JajiSang-Hyun Song alisema kuwa kimsingi kuna mazingira ambayo yanaweza kutumika kumhurusu mshtakiwa kutohudhuria mahakamani wakati wa kesi yake, lakini hata hivyo jambo hilo linategemea na utashi wa mahakama na mfumo wa kesi yenyewe.