Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lafanya mashauriano kuhusu Mali

Baraza la Usalama lafanya mashauriano kuhusu Mali

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limesikiliza ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali nchini Mali, na kufanya mashauriano kuhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSMAH. Joshua Mmali ana taarifa kamili

(TAARIFA YA JOSHUA)

Kikao cha Baraza la Usalama kuhusu Mali kimeanza kwa kusikiliza ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali nchini humo, ambayo imewasilishwa na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu na mkuu wa ujumbe wa MINUSMAH, Bert Koenders.

Katika ripoti hiyo, Bwana Koenders amesema kuwa, matukio ya hivi karibuni ya ghasia katika mwezi Septemba yanatia hofu kuhusu hali ya usalama nchini Mali, na yanapaswa kuwa onyo kwa jamii ya kimataifa.

Amesema kinachohitajika sasa ni kuepukana na vianzo vya matatizo yaliyopo sasa nchini humo, huku akiongeza kuwa licha ya hatua zilizopigwa hivi sasa kisiasa na kufungua milango ya kujikwamua tena kwa Mali, bado changamoto za kibinadamu na maendeleo ni sugu.

Nimeshangazwa na viwango vya utapiamlo nchini humo. Watu wengi walolazimika kuhama na wakimbizi wanarejea nyumbani. Hata hivyo, usaidizi wa kimataifa kwa hali ya dharura ya kibinadamu na utapiamlo nchini Mali haujawa mzuri, kwani ombi la misaada ya kibinadamu limepata ufadhili wa asilimia 37 pekee. Mwezi huu, ambao muhula wa kwanza wa mwaka mpya shuleni unapoanza, mahitaji ya sekta ya elimu ni makubwa hata zaidi. Ni muhimu tusirudie makosa ya zamani, bali tukabiliane na vianzo vya changamoto zilizopo sasa Mali”

Kuhusu majukumu ya ujumbe wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMAH, Bwana Koenders amesema vikosi vya ujumbe huo vinahitaji vifaa zaidi, zikiwemo ndege za helikopta, ili kuweza kutekeleza majukumu yake, hususan la kuwalinda raia katika maeneo ya vijijini.