Waliofariki dunia kwenye ajali ya mashua Lampedusa wafikia 311

11 Oktoba 2013

Imefahamika kuwa zaidi ya wahamiaji 311 walifariki dunia katika ajali ya mashua iliyotokea wiki iliyopita katika kisiwa cha Lampedusa,Italia. George Njogopa na taarifa kamili.

(TAARIFA YA GEORGE NJOGOPA)

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR imesema kuwa wahamiaji wengine 156 wengi wao wakiwa ni raia wa Eritrea waliokolewa na imeelezea ajali hiyo kuwa ni baya zaidi kuwahi kutokeaa katia historia ya ajali kwenye eneo hilo.

UNHCR imesema kuwa imekaribisha hatua iliyotangazwa na kamishna ya Umoja wa Ulaya iliyosema kuwa inachukua hatua za haraka kuzuia kutojirudia tena kwa matukio kama hayo.

Hata hivyo shirika hilo limesema kuwa bado kunahitajika mipango makini zaidi ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji ambao mara zote wamekuwa wakitumia upenyo huo wa kisiwa cha Lampedusa kwa ajili ya kuingia nchi za Ulaya. Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR

 (SAUTI YA ADRIAN EDWARD)

“Kimsingi ni muhimu zaidi kuhakikisha kwamba hatua zote zinachukuliwa ili kutatua mambo ambayo yanasababisha nchi kuzalisha wakimbizi . Lazima kuwe na taarifa za kutosha kuelezea hali ya hatari kwa wahamiaji haramu wanaoingia nchi za Ulaya.Kunahitajiia pia kubadilishana taarifa kuhusiana na njia na mbinu zinazotumika kwa wahamiaji hao."

Aidha UNHCR imesema kuwa karibu wahamiji 30,000 wameingia nchini Italia kutoka eneo la Afrika ya Kaskazini katika kipindi cha January na Septemba mwaka huu.