Rais wa Sudan Kusini ahaidi kushinda vita dhidi ya HIV:

2 Oktoba 2013

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit amesisitiza ahadi yake ya kupanua wigo wa mipango ya kupambana na ukiwmi nchi nzima. Taarifa ya Flora Nducha inafafanua

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Rais Kiir alipokutana na naibu mkurugenzi wa shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi UNAIDS Luiz Loures mjini Juba amesema Sudan Kusini ilishinda vita vya uhuru , pia itashinda vita dhidi ya ukimwi.

Ameongeza kuwa vita hivyo vitakuwa ni kipaumbele chake cha kwanza kwani lengo lake ni kuwalinda watu wake kwa gharama yoyote. Sudan Kusini ilijipatia uhuru kutoka Sudan mwaka 2011 baada ya miaka 30 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilikatili maisha ya watu zaidi ya milioni 2.5.

Juhudi zinahitaji kuongezwa nchini Sudan Kusini katika vita dhidi ya ukimwi. Mwaka 2012 inakadiriwa kuwa watu 150,000 wanaishi na virusi vya HIV na asilimia 9 tuu ya wanaohitaji kupatiwa dawa za kurefusha maisha kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO ndio wanaopata dawa hizo. Na asilimia 13 pekee ya kina mama wajawazito wanaoishi na virusi ndio wanaweza kupata dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huku vifo vya ukimwi vimeongezeka mara mbili kutoka 6900 mwaka 2001 hadi 13000 mwaka 2012.