Ban alaani shambulio lililogharimu maisha ya wanachuo zaidi ya 40 Nigeria.

30 Septemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio katika chuo cha kilimo Kaskazini mwa Nigeria lililosababisha vifo vya wanachuo zaidi ya 40 huku wengine wakijeruhiwa.

Bwana Ban ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na serikali ya watu wa Nigeria kufuatia maafa hayo.

Katibu Mkuu amesikitishwa na mfululizo wa mashambulizi yanayoelekezwa kwa wanafunzi na walimu Kaskazini mwa Nigeria na kutaka kukomeshwa kwa kile alichokiita uhalifu usio na maana na wa kikatili. Amesema vitendo hivyo kamwe havikubaliki.

Bwana Ban kadhalika ametaka wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria haraka na juhudi endelevu zichukuliwe ili kuzuia mashambulizi kama hayo na kuhakikisha usalama kwa raia.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter