Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay ataka haki ya faragha iheshimiwe akiongea kuhusu Snowden

Pillay ataka haki ya faragha iheshimiwe akiongea kuhusu Snowden

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema hali ya raia wa Marekani, Edward Snowden na madai ya ukiukwaji wa haki ya faragha uliotekelezwa na mifumo ya ujasusi inazua masuala kadhaa muhimu kuhusu haki za binadamu za kimataifa.Bi Pillay amesema, ingawa masuala ya usalama wa kimataifa na uhalifu yanaweza kuhalalisha mifumo hiyo ya ujasusi kwa kiasi fulani mahsusi, kusipokuwepo umakini katika kulinda haki ya watu ya faragha, mifumo hii inaweza kuathiri vibaya mno kufurahia kwa haki za binadamu.

Akirejelea aya za 12 na 17 katika azimio la kimataifa kuhusu haki za umma na kisiasa zinazopinga ukiukwaji wa haki ya faragha, Bi Pillay amesema watu wanatakiwa waishi bila hofu ya kwamba mawasiliano yao ya faragha yanasikilizwa na serikali hivi hivi tu.

Amesema haki ya faragha, haki ya kupata habari na uhuru wa kujieleza vinakwenda sambamba, na kwamba raia wana haki ya kidemokrasia ya kushiriki masuala ya umma, na haki hii haiwezi kufurahiwa kwa kutegemea habari zinazoidhinishwa na serikali tu.

Ameongeza kuwa kesi ya Snowden imeonyesha haja ya kuwalinda watu wanaotoa habari kuhusu mambo yanayoathiri haki za binadamu, pamoja na kuhakikisha heshima ya haki ya faragha.

Amesema mifumo ya kitaifa ya sheria inapaswa kuweka njia ya watu wanaotambulisha ukiukwaji wa haki za binadamu kufanya hivyo bila kuogopa kuadhibiwa.