MONUSCO NA UNICEF zaitaka DRC ichunguze ubakaji wa watoto

27 Juni 2013

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC, Roger Meece na Mkuu wa Shirika la Kuwasaidia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, nchini humo, Barbara Bentine, wameelezea kusikitishwa kwao na matukio ya hivi karibuni ya ubakaji wa wasichana wadogo katika maeneo ya Kavumbu na Ruwiro katika mkoa wa Kivu ya Kusini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa katika kipindi cha miezi miwili ilopita, wasichana tisa wenye umri wa kati ya miezi kumi na minane na miaka kumi na miwili wamelazwa katika hospitali ya Panzi Kivu ya Kusini, wakiwa na majeraha ya kudhulumiwa kwenye miili yao, na majeraha mabaya sana ndani ya miili yao, ambayo yamesababisha vifo vya wasichana wawili kati yao.

Kwa mujibu wa UNICEF, matukio haya ya uhalifu yametokana na desturi potovu za kijadi ambazo huenezwa na watu wanaowateka watoto wadogo kutoka kwa jamii zao.

UNICEF na MONUSCO zinasifu hatua ya mamlaka za DRC kuwakamata washukiwa wawili katika uhalifu huo, lakini zinataka hatua hiyo ifuatiwe na hatua za kina za kuchuguza na kuwashtaki wote walohusika katika vitendo hivi vya aibu na unyama, chini ya wajibu wake chini ya sheria ya kitaifa na kimataifa.