Libya isaidiwe kukabiliana na changamoto zilizopo sasa: ICC

8 Mei 2013

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC amelitolea wito Baraza la Usalama kuendelea kuisaidia Libya kuimarisha mifumo yake. Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(Taarifa ya Massoi)

Licha ya kupiga hatua katika urejeshaji wa Libya kwenye mkondo wa demokrasia, heshima ya haki za binadamu na uongozi wa kisheria, bado kuna changamoto nyingi. Hayo yamesemwa na Mwendesha Mashataka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, Fatou Bensouda, wakati akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo limefanya kikao kuhusu hali nchini Libya hii leo.

Bi Bensouda amesema wakati Baraza hilo lilipoamua kupeleka kesi ya Libya kwa mahakama hiyo ya ICC, uamuzi huo ulikuwa kwa ajili kuhakikisha uwajibikaji kwa watendaji uhalifu dhidi ya ubinadamu, na pia kuweka amani na usalama wa kudumu kwa watu wa Libya.

Kwa sababu hiyo, Bi Bensouda ametoa wito kwa Baraza la Usalama liendelee kuisaidia Libya kukabiliana na changamoto inazokumbana nazo sasa, na kwa juhudi hizo za ushirikiano, kuhakikisha haki na amani vinaendelezwa.

"Libya imeonesha kuelewa kikamilifu tofauti kati ya wajibu wa kisiasa wa Baraza hili, na wajibu wa kisheria wa mahakama ya ICC, hata pale Baraza hili limepeleka kesi ya hali ya Libya kwa ICC. Muhimu zaidi ni kwamba Libya inafanya juhudi za kuimarisha mfumo wake wa sheria. Kwa kuendesha kesi zinazohusu ukiukaji wa haki za binadamu kwa washukiwa wote kwa usawa, haki, na uwazi, na kuendelea kuheshimu taratibu za kisheria za mahakama ya ICC, Libya inaweza kuweka mfano wa kudumu utakaoigwa na nchi zingine."

Bi Besnouda amesema, kwa kuzingatia viwango vya uhalifu ulotekelezwa nchini Libya na changamoto zinazoikabili serikali mpya ya Libya, bado wajibu wa mahakama ya ICC yanahitajika ili kuhakikisha uwajibikaji nchini humo kwa watenda uhalifu.