Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Mary Robinson ziarani Rwanda

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Mary Robinson ziarani Rwanda

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukanda wa Maziwa Makuu, Mary Robinson, leo amizuru Rwanda wakati akiendelea na ziara yake ya kikanda, yenye minajili ya kupigia debe utekelezaji wa makubaliano yalotiwa saini na nchi 11, na ambayo ameyaita “makubaliano ya matumaini.”

Makubaliano hayo ambayo yalisainiwa mjini Addis Ababa mnamo Februari 2013, yanalenga kutokomeza mizozo na kuteseka kwa watu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Akiwa Kigali, Bi Robinson amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Paul Kagame, ambaye alikuwa safarini kwenda ngambo. Amekutana pia na Waziri wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo na maafisa wengine wa ngazi za juu, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya umma, makundi ya wanawake, mabalozi na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.

Bi Robinson ameelezea kutiwa moyo na mazungumzo aliokuwa nayo na rais na waziri Mushikiwabo, na kufurahishwa na hakikisho kutoka kwa serikali ya Rwanda kuwa itashirikiana naye kwa karibu ili kuyatekeleza makubaliano ya Addis Ababa.