Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ali Al-Za’tari akaribisha mazungumzo ya amani ya Sudan

Ali Al-Za’tari akaribisha mazungumzo ya amani ya Sudan

Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Ali Al-Za'tari ameungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon katika kukaribisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya Sudan na kundi la Sudan People's Liberation Movement North yanayofanywa chini ya mwavuli wa Jopo la ngazi ya juu ya utekelezaji la Muungano wa Afrika, AUHIP mjini Adis Ababa Ethiopia.

Zaidi ya watu milioni moja wameathiriwa na mgogoro kati y Kordofan Kusini na Blue Nile uliodumu kwa miaka miwili sasa.

Bwana Al-Za'tari amesema kuna haja ya kusimamisha mapigano na kutoa msaada kwa raia wote wahitaji na kuzitaka pande husika katika mgogoro kuendelea na mtizamo chanya wa kutovumilia mateso ya muda mrefu wanayopata raia.

Mwakilishi huyo mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan pia amesema Umoja huo na wabia wake wa misaada ya kibinadamu wako tayari kutoa msaada punde watakapopata uwezo wa kufika katika maeneo husika. Amesema wanahitaji kutoa misaada ya chakula na mingineyo haraka wakati huu ambapo msimu wa mvua umekaribia na pia wanahitaji kupata mbegu na pembejeo kabla ya msimu wa kuotesha haujaanza ili kuhakikisha mavuno kwa raia.

Amewataka wahisani na washirika kusaidia katika kile alichokiita operesheni muhimu ya kibinadamu.