Ukatili wa kijinsia bado tatizo Angola- Pillay

24 Aprili 2013

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Navi Pillay, amesema licha ya hatua za maendeleo zilizopigwa na Angola ikiwa ni miaka kumi baada ya kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, nchi hiyo inapaswa kutokomeza ukatili hususani wa kijinsia unaofanywa na vikosi vya ulinzi na maafisa wa uhamiaji.

Akitoa majuimuisho ya zaiara yake nchini Angola kwa waandishi wa habari mjini Luanda hii leo, Kamishna Pillay amesema anatambua serikali ina wajibu mkubwa katika kulinda mipaka kutokana na lundo la wahamiaji, wengi wao wakiwa na adhma ya kuchimba almasi kinyume cha sheria, lakini amesema zoezi hilo lazima lifanyike kwa kuzingatia haki za binadamu za kimataifa.

Ameongeza kuwa jamii za kiraia zilizo thabiti ni muhumu kwa demokrasia inayokua na tasasi za kiraia bila shaka zinahisi ziko hatarini na hivyo zinafanya kazi katika mazingira ya kudhibitiwa na kuitaka serikali kujihusisha katika mazungumzo na taasisi hizo.

Kuhusu haki za binadamu Kamishna huyo amesema bado kuna matatizo katika dhana ya tafsiri na utekelezaji wa sheria ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika ambapo mara kadhaa askari wamekuwa wakiwakandamiza waandamanaji.

Katika ziara hiyo Pillay alifanya mazungumzo na Rais wa Angola José Eduardo dos Santos, Mawaziri kadhaa wakiwemo wa sheria na haki za binadamu, viongozi wa mahakama ya katiba na walijadili mambo kadhaa ikiwamo uhamiaji holela unaofanywa kupitia mpaka na Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo ambapo pia alitembelea eneo hilo la mpaka.