Msumbiji yatoa chanjo mpya ya watoto dhidi ya numonia

23 Aprili 2013

Nchini Msumbiji hatma ya afya ya watoto dhidi ya magonjwa ya njia ya hewa hususan numonia imeanza kupata mwanga baada ya serikali ya nchi hiyo kuanza kuwapatia watoto chanjo mpya aina ya PCV10.Chanjo hiyo imeanza kutolewa kwa ufadhili wa mashirika mbali mbali ikiwemo ya Umoja wa Mataifa ya UNICEF, WHO na lile la ubia wa kimataifa wa chanjo, GAVI wakati huu ambapo dunia inaadhimisha wiki ya utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa hatari kama vile surua, polio, donda koo na hata magonjwa ya njia ya hewa.

Felicidade Francisco kutoka Wizara ya afya ya Msumbiji amesema utoaji wa chanjo hiyo ni sehemu ya hatua ya serikali ya kufikia lengo la maendeleo la milenia la kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 103 hadi 75 kati ya Elfu Moja ifikapo mwaka 2015 na kwamba wazazi wanajitokeza kwa wingi ili watoto wao wapatiwe chanjo hiyo.