Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Askari waripotiwa kunyanyasa raia huko Kivu Kaskazini

Askari waripotiwa kunyanyasa raia huko Kivu Kaskazini

Usalama wa raia kwenye jimbo la Kivu Kaskazini huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC bado ni wasiwasi mkubwa ambapo raia wanakumbwa na manyanyaso kutoka kwa askari.

Jarida la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa limewakariri wataalamu wa elimu na ulinzi wa mtoto wakitaja manyanyaso hayo kuwa ni pamoja na zaidi ya watoto Elfu Mbili kwenye eneo la Masisi kulazimishwa na askari kulipa fedha pindi wanapokwenda shule.

Halikadhalika shutuma zimeongezeka dhidi ya askari wa FARDC ambao wanadaiwa kuwanyanyasa wakimbizi wa ndani wanaoishi kwenye kambi rasmi kwa kuwatoza kodi, kuwalazimisha kubeba vifaa vya kijeshi au kuwalazimisha wawafanyie kazi.

Habari zaidi zinasema kwenye eneo la Beni watoto 30 wenye umri kati ya miaka 14 na 17 wamepotea tangu tarehe Mosi mwezi huu, ambapo kupotea kwao kunahusishwa na watu wenye silaha kwenye jimbo la Orientale.