Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yahitaji dola Bilioni 1.4 kusaidia watoto wenye mahitaji

UNICEF yahitaji dola Bilioni 1.4 kusaidia watoto wenye mahitaji

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ombi maalum la dola Milioni Moja nukta Nne kwa ajili ya kuokoa watoto wanaokumbwa na madhila kwenye nchi 45 duniani kote kwa mwaka huu wa 2013.

Watoto hao wamejikuta mtegoni kutokana na majanga yanayoendelea kwenye nchi zao ikiwemo migogoro, majanga ya asili na mazingira mengine magumu.

UNICEF imetaja nchi kama vile Syria na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambazo migogoro yao kila wakati inamulikwa na nchi ambazo migogoro imesahaulika kama vile Ethiopa, Chad, Somalia na Yemeni ambako imesema watoto na wanawake bado wanakumbwa na mateso.

Mkurugenzi wa Idara ya programu za dharura kwa UNICEF Ted Chaiban amesema fedha hizo zitatumika kuimarisha mipango ya kukabiliana na majanga, kupunguza madhara ya majanga na hata jamii kuweza kuendelea na maisha baada ya visanga vya namna hiyo.