Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azitaka Israel na Palestina kuandama njia ya amani

Ban azitaka Israel na Palestina kuandama njia ya amani

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, linatazamiwa kupiga kura ya kuamua kuhusu ombi la Palestina la kutaka kuwa na hadhi ya uangalizi bila haki ya kupiga kura katika Baraza hilo. Kura hiyo muhimu inafanyika leo tarehe 29 Novemba, ambayo ni siku ya kimataifa ya kusimama bega kwa bega na watu wa Palestina.

Kabla ya kura hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amewataka WaIsraeli na Wapalestina waachane na dhana ya kutofanya lolote kuhusu hali yao, na kuandama mkondo wa amani kwa ajili ya siku za zijazo.

Bwana Ban amesema, tangu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lipitishe azimio nambari 181 miaka 65 ilopita likipendekeza mpaka uwekwe wa mataifa mawili tofauti, suluhu hilo la kuwepo mataifa mawili bado halijatimizwa. Ameongeza kuwa ziara yake katika Mashariki ya Kati hivi karibuni baada ya machafuko Gaza na Kusini mwa Israel, ilidhihirisha baa litokanalo na kutokuwepo suluhu la kudumu kwa mzozo huo.

Amesema siku hii ni muhimu kwa pande zote mbili, na hasa likizingatiwa ombi la Palestina kuhusu hadhi yake katika Baraza Kuu, na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa pamoja na Israel na Palestina kuongeza maradufu juhudi za kuwezesha amani.