Fedha zaidi zahitajika kukidhi mahitaji ya kibinadamu nchini Syria: OCHA

14 Novemba 2012

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA limesema kadri siku zinavyosonga, mahitaji ya kibinadamu nchini Syria yanaongezeka huku uwezo wa kifedha kukidhi mahitaji hayo ukipungua.

Toleo la leo la jarida la masuala ya kibinadamu la OCHA, limesema watu Milioni nne nchini Syria watahitaji misaada ya kibinadamu mapema mwakani, iwapo hali ya sasa itaendelea.

Idadi hiyo inajumuisha takribani watoto Milioni Mbili na vijana, ambao wengi wao wanakabiliwa na msongo wa kiakili uliotokana na wao kushuhudia ghasia na hata kulazimishwa kukimbia makwao.

Jarida hilo linasema hata idadi ya raia wa Syria wanaotafuta hifadhi nje ya nchi yao itaongezeka na kufikia zaidi ya Laki Saba mapema mwakani.

Hata hivyo OCHA imesema asilimia 51 ya fedha za kusaidia wakimbizi wa Syria ndani ya nchi yao hazijapatikana huku wale walio nje ya nchi yao bado asilimia 35 kukidhi mahitaji.

Ujumbe wa hivi karibni wa OCHA na washirika wake uliotembelea maeneo ya Dera’a, Ar-Raqqa na Homs ulibaini mahitaji ya kibinadamu ni makubwa zaidi kuliko ilivyokadiriwa awali ambapo idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao wanaishi kwenye mazingira magumu ikiwemo mashambani, kwenye mahema na majengo ya umma.

Ujumbe huo umesema kadri msimu wa baridi kali unavyokaribia, wakimbizi hao wanahitaji haraka makazi bora, nguo za kujihifadhi na baridi, mablanketi na vifaa vya kuleta joto.