Jumuiya ya kimataifa ionyeshe inajali eneo la Sahel: Mjumbe wa UM

14 Novemba 2012

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Sahel barani Afrika, Romano Prodi amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuonyesha kuwa inajali eneo hilo ambalo linakumbwa matatizo lukuki ikiwemo ukame, njaa na mzozo huko Mali.

Prodi ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa Italia amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari juu ya madhumuni ya ujumbe wake wa kusaidia nchi za Sahel ambapo amesema jukumu lake kubwa ni kutoa usadizi wa kibinadamu na maendeleo, mambo ambayo amesema iwapo yatakosekana, mgogoro wa Mali hautakuwa na suluhisho.

Prodi amesema hatua ya kwanza ni kuhakikisha kuna umoja ndani ya serikali ya Mali:

"Masuala ya kibinadamu na maendeleo ni ya muda mrefu lakini yanapaswa kushughulikiwa mara moja. Tunapaswa kuonyesha tunajali. Kwa hiyo basi itakuwa jukumu langu kuhangaika kupata fedha, kuhamasisha watu kuchukua maamuzi thabiti juu ya hilo na tayari ninashirikiana na serikali mbali mbali kuanzisha mfuko kwa ajili hiyo.”

Mjumbe huyo maalum amesema ili kupata suluhu la mzozo katika ukanda wa Sahel kuna umuhimu wa kufanya kazi pamoja na pande mbali mbali zinazoshughulika na eneo hilo ukiwemo Umoja wa Afrika, Ufaransa, Uingereza.