Baraza Kuu la UM laitaka Marekani ifute vikwazo dhidi ya Cuba

13 Novemba 2012

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo limepitisha azimio la kuitaka Marekani kufuta vikwazo vyake ilivyoiwekea Cuba mwaka 1962.

Nchi 188 kati ya 193 wanachama wa Baraza hilo leo walipiga kura kuunga mkono azimi hilo huku nchi Tatu ambazo ni Marekani yenyewe, Israel na Palau zikilikataa huku visiwa vya Marshal na shirikisho la Micronesia hazikupiga kura.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodriguez ambaye ndiye alitambulisha azimio hilo amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi yake vimesalia kuwa vyanzo vikuu vya matatizo ya kiuchumi nchini mwake.

"Kama ilivyoelezwa katika ripoti ya Katibu Mkuu, thamani ya athari za kiuchumi zitokanazo na vikwazo hivyo vya miaka 50 ni karibu dola bilioni Sita. Hasara hiyo imethamanishwa kwa kiasi hicho kwa kuzingatia kushuka kwa thamani ya dola ikilinganishwa na bei ya dhahabu. Mtu yeyote mwenye akili timamu anaweza kuona hali ya maisha na kiwango cha maendeleo ambacho Cuba ingalikuwa navyo iwapo fedha hizo zingalikuwepo.”

Halikadhalika amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba ni kinyume na sheria ya kimataifa na pia malengo na misingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.