Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Sudan iharakishe uchunguzi wa ripoti za shambulio huko Sigili: UNAMID

Serikali ya Sudan iharakishe uchunguzi wa ripoti za shambulio huko Sigili: UNAMID

Kaimu Mkuu wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID, Aichatou Mindaoudou ametaka serikali ya Sudan kuharakisha mchakato wa uchunguzi wa ghasia zinazoripotiwa kutokea kijiji cha Sigili.

Ametoa agizo hilo kufuatia ripoti za hivi karibuni zinazodai kuwepo kwa shambulio dhidi ya raia siku ya Ijumaa kwenye kijiji cha Sigili kilichoko kilometa 40 magharibi mwa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Taarifa ya UNAMID inasema kuwa ujumbe huo ulipeleka kikundi cha raia na askari huko Sigili na eneo la Abu Delek ili kuthibitisha ripoti hizo ambapo katika kijiji cha Sigili waliona dalili kuwa kimetelekezwa ghafla, walishuhudia uharibifu wa nyumba na mali, wanyama waliouawa, na hata silaha kwenye kijiji hicho.

Hata hivyo hawakuweza kufika eneo la Abu Delek kwa sababu wakiwa njia msafara wao ulisimamishwa na kikundi kimoja cha waasi kilichokata kuwakagua na baada ya mjadala mrefu wachunguzi hao waliamua kusitisha safari yao.

Bi. Mindaoudou amezitaka jamii zote huko Darfur kujizuia kufanya vurugu ambazo zimesababisha machungu na vifo kwenye eneo hilo.