Makao makuu ya idara ya uhamiaji yafunguliwa Somaliland

6 Novemba 2012

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM limezindua makao makuu mapya ya idara ya uhamiaji katika mji mkuu wa Somaliland Hargeisa. Mradi huu unatarajiwa kuwezesha idara ya uhamiaji eneo la Somaliland kutoa usimamizi wa mipaka unaohitajika.

Uzinduzi wa makao hayo ulihudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu serikalini wakiongozwa na rais wa Somaliland Ahmed Mohamed Mohamoud (Siilaanyo). Jengo hilo la gharama ya dola 250,000 lililofadhiliwa na serikali ya Japan pia litakuwa na ofisi za kusajili na kutoa pasipoti na ukusanyaji wa takwimu.

Ubalozi wa Japan nchini Kenya unasema kuwa Japan iko tayari kuchangia kwenye ujenzi wa taifa la Somalia na kufanya kazi na washirika wote yakiwemo maeneo ya Somaliland na Puntland.