Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama libadili makubaliano kuwa azimio ili kumaliza mzozo Syria: Brahimi

Baraza la Usalama libadili makubaliano kuwa azimio ili kumaliza mzozo Syria: Brahimi

Mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu, Lakhdar Brahimi amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa libadilishe kuwa azimio, makubaliano ya mwezi Juni kuhusu hatua za kuweka kipindi cha mpito nchini Syria kwa lengo la kusaidia kumaliza mzozo unaoendelea nchini humo.

Brahimi amesema hayo leo huko Cairo, Misri wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amerejelea kauli yake kuwa mgogoro wa Syria hauwezi kumalizika kwa njia ya kijeshi bali suluhisho pekee ni la kisiasa kupitia mchakato utaokubaliwa na pande zote.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bwana Brahimi ametaka nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ziendelee na mazungumzo ili makubaliano hayo yaliyopitishwa mjini Geneva na kundi kuhusu Syria linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa yaweze kubadilishwa kuwa azimio.

Akiwa Cairo katika harakati za kupatia suluhu mgogoro wa Syria, Brahimi alikuwa na mazungumzo jana usiku na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov na Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu, Nabil El-Araby.