Ofisi ya uchunguzi dhidi ya ugaidi ipewe mamlaka zaidi: Emmerson

2 Novemba 2012

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na utetezi wa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza wakati wa harakati zozote za kupinga ugaidi, Ben Emmerson amelitaka Baraza la Usalama la Umoja huo kuhakikisha vikwazo vyake dhidi ya kikundi cha kigaidi cha Al Qaeda vinazingatia haki za binadamu.

Emmerson amesema hayo leo mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati akiwasilisha ripoti yake kuhusu mamlaka ya ofisi ya uchunguzi dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu, jinsi inavyozingatia haki hizo na athari za mchakato wake kwenye matatizo yaliyobainika kutokana na vikwazo dhidi ya kikundi cha Al Qaeda.

Amesema utaratibu wa vikwazo ulioanzishwa na Baraza la Usalama mwaka 1999, uliipatia kamati ya vikwazo ya baraza hilo wezo wa kuainisha orodha ya watu na taasisi zinazotuhumiwa kwa ugaidi lakini kamati hiyo haipitii ushahidi kutathmini orodha hiyo.

Mtaalamu huyo amesema pindi mtu au taasisi inapokuwa kwenye orodha hiyo, hukumbwa na madhila ikiwemo kunyimwa haki kadhaa ikiwemo ile ya faragha na kusafiri jambo ambalo amesema linafanya Baraza la usalama kujigeuza kuwa chombo cha kisheria na kimahakama.

Badala yake Emmerson ametaka ofisi ya huru ya uchunguzi wa vikwazo dhidi ya Al Qaeda iliyoanzishwa mwaka 2009 inapaswa kupewa mamlaka ya kufanya maamuzi ambayo kwa sasa iko ndani ya kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama.