Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yasema misaada ya chakula na malazi yahitajika haraka Rakhine

UNHCR yasema misaada ya chakula na malazi yahitajika haraka Rakhine

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema wafanyakazi wake wameweza kufika katika vijiji vilivyokumbwa na mapigano kwenye jimbo la Rakhine, magharibi mwa Myanmar ambako serikali ya nchi hiyo imesema watu 35, 000 wamepoteza makazi kutokana na vurugu hizo za hivi karibuni.

Msemaji wa UNHCR Adrian Edwards, amesema ziara ya wafanyakazi hao inafuatia ruhusa ya serikali ambapo walitembelea vijiji kadhaa kwenye vitongoji vya Myebon, Mrauk-U and Minbya jimboni humo. Amesema wamebaini kuwa wakazi wa vijiji hivyo wanahitaji msaada wa haraka chakula na malazi na idadi kubwa ya watoto waliochwa peke yao wakati wa vurugu wana utapiamlo..

Edwards amesema watumishi wa afya waliweza kutoa huduma mbali mbali ikiwemo ya matibabu kwa wanawake 14 ambao wamesema kujifungua kwao kulichochewa na ghasia na kwamba wanakabiliwa na matatizo kunyonyesha watoto wao wachanga.

Katika vijiji hivyo wafanyakazi hao wa UNHCR walishuhudia pia uwepo wa polisi na askari wa jeshi na wanavijiji walieleza wanahofia usalama wao iwapo askari hao wataondoka.