Ban ataka vurugu huko Rakhine, Myanmar zikomeshwe

26 Oktoba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon ametaka vurugu zilizoanza upya kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar zikomeshwe mara moja na amezisihi mamlaka nchini humo kuchukua hatua kumaliza vurugu hizo.

Ban amesema hayo kupitia kwa msemaji wake wakati huu ambapo vurugu hizo zimesababisha vifo vya wat 56 na majeruhi kadhaa na nyumba kuchomwa moto.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema anatambua utashi wa kisiasa wa hali ya juu nchini Myanmar wa kumaliza mzozo huo baina ya jamii tofauti lakini amesema kitendo cha kuvunja sheria ni lazima kidhibitiwe mara mora. Vurugu hizo katika vitongoji vitano vya jimbo hilo la Rakhine zimeelezewa na Katibu Mkuu Ban kuwa zinasikitisha na zimeibuka miezi minne baada ya vurugu za mwezi Juni kati ya waumini wa kibuda na waislamu wa Rohingya zilizosababisha serikali ya nchi hiyo kutangaza hali ya hatari kwenye jimbo hilo.

Bwana Ban amesema wanamgambo na wahalifu wanatumia vibaya kuongezeka kwa kutokuaminiana kati ya jamii hizo na kusababisha vifo, uharibifu wa mali, familia kupoteza makazi na hata hofu, chuki na manyanyaso kwa watu mbali mbali.

Mapema mwezi huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi lilieleza kuwa idadi ya watu waliopoteza makazi kwenye jimbo la Rakhine inazidi kuongezeka ambapo Elfu Sabini na Watano wanaishi kwenye kambi huku wengine zaidi wakihitaji misaada ya kibinadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud