Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa haki za binadamu kwenye UM alaani mashambulizi ya msafara wa UM Darfur

Mkuu wa haki za binadamu kwenye UM alaani mashambulizi ya msafara wa UM Darfur

Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Ravina Shamsadani amelaani vikali mashambulizi ya siku ya Jumatano Kaskazini mwa Darfur shambulizi yaliyolenga msafara wa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, polisi , wafanyikazi wa Umoja wa Matifa pamoja na maafisa wawili wa haki za binadamu.Msafara wa kikosi cha Pamoja cha Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika UNAMID ulikuwa ukielekea kwenye kijiji cha Hashaba kaskazini mashariki mwa wilaya ya Kutum kuchunguza ripoti za mauaji ya raia 70 kwenye kijiji hicho mwezi uliopita.

Mlinda usalama mmoja kutoka Afrika Kusini aliuawa wakati msafara wao uliposhambuliwa na watatu kujeruhiwa. Shambulizi hilo linafikisha idadi ya walinda usalama waliouawa mwezi huu kuwa watano. Walinda usalama 43 wameuawa taangu kubuniwa kwa kikosi cha UNAMID mwezi Disemba mwaka 2007. Ravina Shamdasani ni afisa kutoka Ofisi ya Masuala ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa.

Tunalaani vikali shambulizi la siku ya Jumatano kaskazini mwa Darfur dhidi ya msafara wa Umoja wa Mataifa wakiwemo wanajeshi , polisi , wafanyikzi na pia maafisa wawili wa haki za binadamu. Tunaikumbusha serikali ya Sudan kuwa ina wajibu wa kulinda wafanyikazi wa UNAMID wanapotekeleza majukumu yao ya kuwalinda raia na kufuatilia ukiukaji wa haki za binadamu. Serikali ni lazima ianzisha uchunguzi wenye lengo la kuwafikisha mahakamani wahusika . Kuna mahitaji ya dhararua ya kumaliza ukwepaji wa sheria Darfur unaosababisha mashambulizi kama hayo.”