Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yaanzisha mafunzo ya madhara ya vita kisaikolojia na kijamii nchini Libya

IOM yaanzisha mafunzo ya madhara ya vita kisaikolojia na kijamii nchini Libya

Kundi la wataalamu 35 wa afya, elimu na jamii limekuwa la kwanza kujiunga na kozi ya madhara ya vita kisaikolojia na kijamii iliyoanzishwa na shirika la kimataifa la Uhamiaji, IOM kwenye chuo kikuu cha Tripoli nchini Libya kwa msaada wa Italia.

Kozi hiyo ya miezi sita itawapatia mafunzo wataalamu hao ambao watawasaidia watu waliopata madhara ya kisaikolojia na kijamii kutokana na mgogoro nchini Libya na ni sehemu ya mpango wa IOM ya kusaidia waathirika wa mgogoro nchini humo kama ilivyokuwa nchini Lebanon.

Mkuu wa kitengo cha IOM kinachohusika na usaidizi wa athari za kisaikolojia na kijamii, Guglielmo Schinina amesema mpango huo ni muhimu kwa kuwa mara nyingi migogoro inapomalizika mashirika ya misaada huwaacha waathirika wakati ukweli ni kwamba unapomalizika mgogoro wa nje, ndipo mgogoro wa kifikra unapoanza ndani ya raia.

Amesema raia walioshuhudia mauaji hupatwa na msongo na kujihisi kukosa ulinzi na kwamba bila msaada, watu wa aina hiyo ikiwemo raia wa Libya wanaweza kupata madhara makubwa yatakayoathiri jamii.

Asilimia Hamsini ya watu Elfu Tatu mia Tatu walioshiriki utafiti wa IOM kwenye miji ya Tripoli, Benghazi na Misrata walisema wanahitaji msaada wa kisaikolojia huku asilimia Sitini wakisema kuwa maisha yao ya kijamii yamekuwa magumu zaidi baada ya vita.